Jinsi ya mwanamke kujikomboa na dimbwi la umasikini: jifunze nami

Ikiwa leo ni siku ya wanawake duniani leo nimewaandalia makala fupi itakayo kuondoa katika janga la umasikini na kuaacha kuaendelea kuwa ombaomba kwa mwanaume/mpenzi wako

Kama wewe ni mmojawapo wa wanawake wanaohitaji kutengeneza utajiri mkubwa wa kudumu na kuishi maisha yenye uhuru wa kifedha katika maisha yao yote ni vizuri usome hapa. Ila kama wewe ni miongoni mwa wanawake walio tayari kuendelea kuishi maisha ya umasikini pasipo na nia ya dhati ya kuondokana nao, ni vyema nikushauri usisome hapa kwa sababu unaweza kubadilika moja kwa moja na maisha yako yakawa tofauti na namna unavyotaka. Niliwahi kusema, “Kuwa tajiri si dhambi bali kuwa masikini ni kuchagua.” Hivyo basi uchaguzi ni wako kuendelea kuishi katika hali ya umasikini kwa hofu ya kuamua kuchagua kuwa miongoni mwa matajiri, au kuchagua utajiri kama sehemu pekee ya kukupa nafasi ya kuwa huru kiuchumi.

Robert Kiyosaki mwalimu na mtaalamu wa masuala ya fedha na uwekezaji nchini Marekani aliwahi kuandika katika kitabu chake maarufu sana cha masuala ya fedha cha Rich Dad Poor Dad akisema, “There is more than one way to become rich” (Kuna njia zaidi ya moja ya kuwa tajiri). Kama kuna njia zaidi ya moja ya kuwa tajiri maana yake uamuzi ni wako wa wewe kuchagua njia mojawapo inayoweza kuwa salama na halali kwako kwa ajili ya kukupeleka katika utajiri kama unavyotaka. Nataka nikuambie zipo njia zilizo halali na njia zisizo halali katika kukupatia utajiri, katika makala hii sipo kwa ajili ya kukupa njia zisizo halali bali nataka kukupa njia zilizo sahihi na halali kwako ambazo ndio zilizotumika na matajiri wengi leo hii hadi kufikia mahali walipofikia sasa.

Siri 7 Za kukupeleka katika utajiri wa kudumu na kuondokana na maisha ya umasikini.

1: Miliki biashara yako binafsi au kuwa mwekezaji.

Nataka nikuambie wazi kuwa usijaribu sana kuwaza utajiri mkubwa nje ya kumiliki biashara yako binafsi. Utafiti unaonyesha wazi asilimia 85 hadi 90 ya matajiri wengi duniani ni watu wenye kumiliki biashara zao binafsi. Hii inaonyesha wazi ni ngumu sana kuwa tajiri au kuwa na uhuru wa kifedha kama bado utaendelea kuwa chini ya mtu au kampuni fulani kama mwajiriwa. Wewe mwenyewe una ushahidi wa kutosha katika hili, angalia matajiri watano wakubwa unaowafahamu kwa kuchukua mfano wa nchi yetu wanaotajwa na jarida la forbes mara kwa mara kama vile Mohamed Dewji, Rostam Aziz, Salim Bakhresa, Regnald Mengi, Yusuph Manji, na wengineo. Wengi wa matajiri hawa ni wamiliki wa biashara zao na pia ni watu walioamua kuwekeza kwenye biashara mbalimbali kubwa ingawa kila mmoja alianzia chini sana.

Nakusihi hata kama umeajiriwa na wewe ni miongoni mwa watu wanaotamani sana kuwa kwenye uhuru wa kifedha na kutengeneza utajiri mkubwa maishani mwao, amua leo hii kuanzisha hata biashara ndogo ndogo unayoweza kuanza nayo kama biashara yako ya pembeni huku ukiendelea na ajira yako hadi pale biashara uliyonayo itakapokuwa kwa kiwango fulani na hapo unaweza kuamua kuacha kuajiriwa na kuamua kujikita zaidi katika biashara yako uliyoanzisha. Nakushauri kabla ya kuanzisha biashara ni muhimu sana usome soko, kwani kuanzisha biashara pasipo kusoma soko la bidhaa au huduma unayoenda kutoa ni kuamua kupoteza muda, nguvu na fedha zako unazowekeza katika biashara hiyo. Soko ni jambo la muhimu sana (first priority) kabla hujaanzisha biashara yoyote ile unayotaka kuanzisha ni muhimu kusoma soko lake.

2: Tengeneza Mtandao wako wa Mahusiano hasa wa kibiashara

Napenda sana kunukuu baadhi ya maneno ya Bwana Donald Trump mgombea urais nchini Marekani kwa sasa, hii ni kwa sababu ni mtu niliyewahi kusoma vitabu vyake vingi sana alivyoandika ambavyo kwa sehemu kubwa vinahusu masuala ya kibiashara, mojawapo ya kitabu chake cha kwanza kabisa kutoa na alichowahi kuandika cha ‘The Art of the Deal” aliwahi kusema, “You can’t do a good deal with a bad partiner.” (huwezi kuingia makubaliano mazuri na mbia mbaya au hasiyefaa) sentensi hii utaikuta kwenye kitabu cha “Midas Touch” ambapo Robert Kiyosaki anairudia pia. Huwezi kufanya biashara na mtu hasiyefaa.

Kama unahitaji kufanya biashara na biashara hiyo kukua na kukupa faida kubwa zaidi siku hadi siku inakubidi utengeneze mtandao wa kutosha na watu wengine wanaofanya biashara. Kuna msemo unaosema, kama mtu anahitaji kuwa daktari ni vizuri akae na madaktari ili aweze kujifunza zaidi kutoka kwao namna ya kuwa daktari. Jambo hili utalikuta pia hata katika biashara, kama unahitaji kuwa mfanyabishara mwenye mafanikio makubwa katika biashara yako ni muhimu sana kuwa karibu na watu waliokutangulia katika biashara kabla yako. Kaa na watu wanaofanya biashara na waliofanikiwa katika biashara ili waweze kukupa mbinu wanazozifahamu kuhusu biashara na hapo utakuwa unajiweka katika mazingira mazuri ya kufanikiwa zaidi.

3: Wekeza katika Elimu ya fedha.

Kati ya jambo linalowazuia watu wengi sana kufanikiwa hata wanaopata fedha nyingi kwa wakati fulani na badae kujikuta hawaoni fedha zile, ni kukosa utaratibu wa matumizi na uongozi mzuri wa fedha wanazozipata unaoweza kuwa na faida kwao wa kuwaletea mafanikio na utajiri mkubwa maishani mwao. Hata kama utakuwa na biashara yenye kukuingizia faida kubwa kiasi gani kwa siku au mwezi, lakini kama hautokuwa makini kujua namna ya kutawala hisia zako juu ya matumizi yako ya fedha ni vigumu sana kutengeneza utajiri mkubwa maishani mwako. Jiulize swali hili, Je, huwa ukipata faida kwenye biashara yako ni asilimia ngapi unayoirudisha katika biashara yako au kutumia katika kuwekeza?

Watu wengi sana wanazani utajiri unatengenezwa kwa kufahamu mambo mengi, kusoma vitabu vingi au kuwa na elimu kubwa ya chuo kikuu, Hapana. Nataka nikuambie elimu unayoipata chuoni au mahali popote pale ni muhimu sana kama utakapoamua kutumia maarifa yale unayoyapata kufanikiwa kwenye maisha yako. Elimu isiyo na faida kwako binafsi haina maana ya kuichukua. Kama unahitaji kutengeneza utajiri wa kudumu kwenye maisha yako ni muhimu zaidi kuwekeza kwanza kwenye elimu ya fedha. Amua kujifunza masuala ya uongozi wa fedha, namna ya kukopa na kurejesha, namna ya kuingia mikataba mikubwa, namna ya kuzungusha fedha na kuzalisha faida, nakadhalika. Mambo haya unahitaji kujifunza kila mara hata kama si kwa kuingia darasani kwa mara nyingine lakini unaweza kusoma vitabu vilivyoandikwa na watu wengine waliofanikiwa kama kina Emilian Busara, Uebert Angel n.k

4: Tafuta taarifa sahihi.

Wapo watu wanaona kama utajiri si sehemu ya maisha yao ni sehemu ya watu fulani tu, hivyo wao hawapaswi hata kufikiri kuhusu mambo hayo. Kama wewe ni mmojawapo wa watu hao najua si kosa lako, bali ni kosa la taarifa zilioingia akilini mwako miaka kadhaa iliyopita tangu hapo awali kwenye makuzi yako. Yupo rafiki yangu mmoja ambaye ni mtaalamu katika kufundisha masomo ya namna ya kubadili chanzo chako cha taarifa 
Fred Msungu aliwahi kusema, “Wewe ni matokeo ya muono wako wa ndani na kesho yako inaathiriwa sana na lile tamanio au ono lako la ndani, na baada ya kuona ni lazima uchukue hatua za kuanza kuitengeneza ile picha ya ndani itokee kwenye ulimwengu halisia.”

Fred Msungu anaendelea kusema, “Kuona peke yake haitoshi! Njia rahisi ya kutambua unaona nini ndani yako! Chunguza aina ya habari unazopenda, magazeti unayosoma, movie unazozipenda. Chunguza aina ya watu uliowafuta (follow) kwenye instagram, facebook, snapchat, nakadhalika. Angalia aina ya watu au marafiki waliokuzunguka muda huu. Angalia katika computer au simu yako ni nini kina GB kubwa kuliko vingine vilivyomo. Ukishapata jibu la maswali yote haya ujue HUYO NDIO WEWE. Hakuna namna utakua tofauti na aina ya taarifa unazoziingiza kichwani…..kama vile ambavyo chakula unachokula kinaamua AFYA yako …basi ndivyo taarifa inavyoathiri maisha yako.”(mwisho wa kunukuu). Kama unahitaji kuwa tajiri ni sharti ubadili chanzo chako cha taarifa na watu waliokuzunguka. Huwezi kutegemea kuwa tajiri mkubwa huku muda mrefu unazungukwa na watu wanaowaza mawazo hasi (mawazo ya kushindwa) juu ya maisha yao. Huwezi kuwa tajiri kama muda wote mambo unayoangalia na kusoma ni yale ya udaku badala ya kufatilia taarifa sahihi zinazoweza kukuongezea mawazo mapya ya kutengeneza fursa mpya za kibiashara.

5: Jifunze namna ya kuuza.

Kila mtu ni muuzaji katika dunia hii tangu hapo alipozaliwa. Kuna kitu unachouza, kile kilichokufanya uje duniani ndio mtaji wako na ndicho unachotakiwa ukiuze ili kilete matokeo makubwa katika maisha yako. Huwezi kufanikiwa katika maisha na kutengeneza utajiri mkubwa kama huwezi kujifunza namna ya kutoa au kuuza, kwani kwa kadiri unavyouza au kutoa ndivyo unavyozidi kutengeneza faida na kukuza mtaji wako zaidi. Ndio maana elimu ya kuuza ni elimu muhimu sana na ni elimu ya pili baada ya ile ya fedha inayoweza kukusaidia kutengeneza utajiri mkubwa katika maisha yako.

Usipojua namna ya kutetea bidhaa au huduma yako unaiyotoa kwa wateja, namna ya kuvutia wateja kununua bidhaa zako unazotengeneza na zaidi namna ya kutengeneza jina lako (Brand) kwa kupitia kile unachokifanya, basi elewa ni vigumu sana kutengeneza utajiri mkubwa kwa kupitia biashara yako unayoifanya. Ni muhimu sana kuwekeza pia katika elimu ya mauzo na namna ya kuuza ili uweze kunufaika na kutengeneza utajiri mkubwa na wa kudumu kupitia kitu unachokitoa kwa wanunuaji wako.

6: Usiogope kukataliwa mara nyingi.

Nimewahi kusoma habari na shuhuda nyingi sana za watu waliofanikiwa na kutengeneza utajiri mkubwa kwenye maisha yao na vizazi vyao. Katika kusoma kote shuhuda za watu hao sikuwahi kuona mtu aliyewahi kuwa tajiri kwa njia halisi au kufikia mafanikio makubwa kabla hajapitia kukataliwa
Wapo wengi waliokataliwa lakini leo hi ni mataji kama
 Oprah Winfrey’s, Jack Ma, na wengine wengi sana. Usiogope kukataliwa kwani ni sehemu ya maisha.

7: Shikilia na kuishi ndoto yako.

Yawezekana unataka kuwa mfanyabishara na mwekezaji mkubwa, una ndoto ya kuwa daktari, una ndoto ya kuwa mwandisi, nakadhalika kwa eneo unalotaka. Ndoto yako ni muhimu sana katika kukuletea mafanikio makubwa na kukutengenezea utajiri mkubwa kwenye maisha yako kama itafika mahali utaiheshimu na kuitumia kama eneo muhimu la kusaidia wengine.

Ni muhimu sana kuhakikisha una ndoto inayoweza kujibu maswali ya watu wengi katika jamii yako iliyokuzunguka, ili ndoto hiyo iweze kurudisha faida kubwa kwako na hapo ndipo penye nafasi kubwa kwako kwa ajili ya kutengeneza utajiri mkubwa maishani mwako. Usijaribu kuwa na ndoto inayokunufaisha wewe tu, ndoto maana yake iwe na faida kwako na kwa wale waliomzunguka.

Ndoto isiyojibu majibu ya watu haina thamani ndani yake – Christopher Mwakasege

Nakupenda sana na huu ni wakati wetu pamoja kutengeneza utajiri mkubwa na kuzidisha matajiri katika kizazi chetu hiki tulichonacho kama nchi nyingine kubwa duniani na ili kuepuka utegemezi katika mataifa makubwa. Uamuzi ni wako kuendelea kuishi katika umasikini au kutumia mbinu hizi kwa ajili ya kujikwamua kimaisha na kuwa na uhuru wa kifedha katika maisha yako yote. Hadi kufikia hapo nakutakia siku njema yenye furaha na uzima katika maisha yako. Karibu ukiendelea kutembelea mtandao huu kila siku kwa ajili ya kujifunza zaidi

Badili maisha yako kabla ya maisha hayajakubadilisha

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

ATHARI 8 ZISABABISHWAZO NA MSONGO WA MAWAZO

HAYA NDIO MAKUNDI 16 YA WATU NA TABIA ZAO

JINSI YA KUPIKA ROST YA NYAMA